Jaribio la mapinduzi lililofanywa na wanajeshi waasi nchini Burkina-Faso linaelekea kushindwa kufuatia vikosi vya wanajeshi watiifu kwa serikali kufanikiwa kuingia katika mji mkuu wanchi hiyo Ouagadougou.
Hatua hiyo inafuatia pia kuachiwa kwa Waziri Mkuu wa serikali ya mpito ambaye alikuwa na anashikiliwa tangu Jumatano iliyopita, Luteni Kanali Yacouba Isaac Zida, pamoja na rais wa serikali hiyo ya mpito kabla haijavunjwa.
Duru kutoka nchini humo zinaarifu kuwa wanajeshi waasi walikuwa wamepewa muda hadi wa saa nne asubuhi hii leo kujisalimisha pasipo kumwaga damu na kurejea katika makambi yao pasipo kuleta madhara ya aina yoyote.
Hapo jana, jeshi la nchi hiyo lilisema ya kuwa lilikuwa linawapeleka wanajeshi wake toka maeneo yote ya nchi hiyo katika mji mkuu wa nchi hiyo Ougadougou hatua ambayo pia ilionekana kuungwa mkono na wanachi wengi wa nchi hiyo walionekana kushangilia baada ya kuwaona wanajeshi watiifu kwa serkali mitaani.
Kiongozi wa mapinduzi aahidi kurejesha madaraka kwa serikali ya mpito
Kiongozi wa mapinduzi hayo, Jenerali Gilbert Diendere, baadaye aliomba radhi kwa taifa hilo kwa njia ya maandishi na akaahidi kurejesha madaraka kwa serikali ya kiraia ya mpito.
Wapatanishi kutoka Afrika magharibi walikuwa wamependekeza kubaliana na hatua ya kiongozi wa mapinduzi kukabidhi madaraka na pia kurejeshwa kwa kiongozi wa serikali ya mpito Michael Kafando mdarakani hadi hapo uchaguzi utakapoitishwa. Kafando ambaye tayari ameachiwa huru na wanajeshi hao waasi kwa sasa amekuwa akiishi katika makazi ya balozi wa Ufaransa mjini Ougadougou.
Uchaguzi nchini humo unatarajiwa kufanyika kabla ya mwezi Novemba mwaka huu na wafuasi wa Rais wazamani wa nchi hiyo Blaise Comapaore wataruhusiwa kushiriki.
Sheria ya uchaguzi iliyopitishwa mwaka huu ilikuwa inawanyima nafasi wafuasi wa chama cha Blaise Compaore kutoshiriki uchaguzi huo.
Compaore aliondolewa madarakani kwa nguvu mwezi Octoba mwaka jana baada ya miaka 27 ya kuwepo madarakani baada ya kujaribu kutaka kuongeza muhura mwingine wa uongozi kwa kubadilisha katiba ya nchi hiyo.
Rais wa Ufaransa Francoise Hollande naye pia aliwataka wale wote waliohusika na mapinduzi hayo kujisalimisha na kukabidhi madaraka kwa mamlaka halali vinginevyo wawe tayari kwa hatua yoyote itakayo fuata.
Alionya pia kuwa Ufaransa ambayo bado ina ushawishi ndani ya taifa hilo ambalo ni koloni lake la zamani inaweza ikachukua hatua ya vikwazo dhidi ya wale wote wanaopinga kufanyika kwa uchaguzi.
Wito wa aina hiyo pia ulitolewa na Marais wa Niger na Chad ambao waliwataka wanajeshi waasi kurejea kambini na kurejesha madaraka kwa serikali ya mpito waliyipindua juma lililopita.