baada ya muda wa mwisho kupita.
Wizara ya mambo ya kigeni ya Misri imesema inafanya juhudi za hali ya juu kumtafuta Tomislav Salopek , mfanyakazi wa kampuni ya kigeni ya utafutaji wa mafuta mwenye umri wa miaka 31 aliyetekwa nyara mwezi uliopita.
Slopek ameonekana katika ukanda wa video wa kundi hilo la IS uliotolewa katika mtandao wa Internet siku ya Jumatano, akiwa amepiga magoti karibu na mtu aliyejifunika uso akiwa ameshika kisu.
Alisoma kikaratasi kwamba watekaji nyara wake watamuua katika muda wa saa 48 iwapo serikali ya Misri itashindwa kuwaachia huru wanawake walioko magerezani, sharti kuu la wanamgambo hao wa Kiislamu katika muda wa miaka miwili iliyopita.
Video hiyo haikufafanua ni wakati gani muda huo wa mwisho ulianzia, lakini zaidi ya masaa 48 yamepita tangu video hiyo kuwekwa mtandaoni, na hakuna taarifa mapema leo Jumamosi juu ya iwapo hatua ya kuuwawa mtu huyo imetekelezwa.
Raia wa kigeni wanahofu
Utekaji nyara huo ambao haukutarajiwa nchini Misri -- umewatisha raia wa kigeni wanaofanyakazi katika makampuni ya kimataifa na kuonesha uwezo wa makundi ya Jihadi , licha ya kampeni kubwa ya kijeshi dhidi ya kundi hilo la IS.
Licha ya kuwa imekuwa ikipambana na wapiganaji wa IS katika eneo hilo la rasi ya Sinai linaloishi watu wachache, taifa hilo la Afrika kaskazini limekuwa halijakumbana na kadhia ya utekaji nyara wa raia wa kigeni na mauaji ya kinyama yanayofanywa na wapiganaji wa jihadi nchini Syria na Libya.
Baba yake Salopek ametoa wito kwa wateka nyara kumwachia mwanae , baba wa watoto wawili, wakati waziri wa mambo ya kigeni wa Croatia Vesna Pusic amesafiri kwenda Cairo kwa mazungumzo ya dharura.
"Nawaomba watu ambao wanamshikilia mwanangu kumruhusu arejee katika familia yake, kwasababu nia yake kwenda katika nchi yenu ilikuwa tu ni kwa madhumuni ya kupata riziki yake na watoto wake.
Hakuna zaidi," Zlatko Salopek ameliambia shirika la habari la AFP nyumbani kwake katika mji wa mashariki nchini Croatia wa Vrpolje.
Waziri wa Croatia aenda Misri
Baada ya mazungumzo kati ya waziri wa mambo ya kigeni wa Misri Sameh Shoukry na Pusic , serikali ya Misri imesema: "Hatutasita kuchukua hatua yoyote kumtafuta na kumpata mateka huyo na uhakika wa usalama wake."
Maelfu ya watu , wengi wao wafuasi wa mrengo wa Kiislamu , wamefungwa jela tangu jeshi kumpindua kutoka madarakani rais mwenye msimamo wa itikadi ya dini ya Kiislamu Mohammed Mursi mwaka 2013 na kuanzisha ukandamizaji uliosababisha vifo kwa waungaji wake mkono.
Salopek alitekwa nyara mwezi uliopita katika barabara kutoka magharibi ya Cairo. Dereva wake ameachiwa bila kudhurika , na polisi imesema wamemhoji.
Katika mji anakotoka Salopek , majirani wanasubiri taarifa kuhusu Salopek , wakimweleza kuwa ni kijana mcheshi.
Chanzo: DW Swahili