Friday, August 07, 2015

Mapigano ya kikabila yauwa zaidi ya 300 Kenya 2015

No comments


Wakati matumizi ya nguvu kati ya makundi yanayohasimiana ni jambo la kawaida katika mikoa ya Bonde la Ufa kaskazini mwa Kenya idadi ya watu waliopoteza maisha yao katika kipindi cha miezi sita ya kwanza ya mwaka huu tayari imefikia kiwango cha jumla cha vifo vilivyotokea kwa mwaka mzima wa 2014.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoratibu masuala ya Kibinaadamu imesema katika taarifa vurugu za matumizi ya nguvu baina ya jamii za kikabila zinaendelea kuzagaa katika Bonde la Ufa kaskazini.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo kuanzia Januari Mosi hadi Juni 30 mwaka 2015 watu 310 wamepoteza maisha yao wengine 195 wamejeruhiwa na 216,294 wamepotezewa makaazi yao ikiwa ni matokeo ya mizozo ya mpakani iliokosa ufumbuzi, wizi wa mifugo na mashambulizi ya kulipiza kisasi,kugombania ardhi na rasilmali za maji na mizozo ya kisiasa.

Uhaba wa rasilmali

Uhasimu kati ya jamii za wafugaji zenye kugombania rasimali haba za mifugo na maji unazidi kupaliliwa kwa kupatikana kwa urahisi bunduki za rashasha na kutokuwepo kwa vyombo vya usalama vya taifa katika maeneo hayo.

Maeneo yalioathirika zaidi ni mikoa ya kaskazini ya Turkana,Baringo,Samburu; Marsabit na Isiolo.

Machafuko mabaya kabisa yalikuwa ni yale kati ya jamii ya Pokot na Turkana halikadhalika kati ya watu wa Turkana na Wasamburu.

Hapo mwezi wa Mei takriban watu 75 waliuwawa katika kipindi cha siku nne cha wizi wa mifugo na mashambulizi ya kulipiza kisasi.Kwa muijibu wa Umoja wa Mataifa hapo mwaka 2014 watu 310 wameuwawa ,214 wamejeruhiwa na 220,000 wamepotezewa makaazi.

Matembezi ya amani

Repoti hiyo inakuja wakati wanariadha kadhaa mashuhuri wa Kenya wakiwemo mabingwa wa zamani wa mbio za marathon Wilson Kipsang na Tegla Loroupe wakielekea kumalizia matembezi yao ya amani dhidi ya matumizi ya nguvu ya kikabila.

Bingwa wa zamani wa marathon katika mashindano ya Jumuiya ya Madola John Kelai mmojawapo wa waandaaji wa matembezi hayo ya kilomita 480 pia anashiriki kuwakumbuka wajomba zake watatu waliouawa katika wizi wa mifugo.

Gwiji wa riadha wa Ethiopia Haile Gebrselassie ajajiunga na matemebezi hayo wakati yakimalizia siku yake ya 22 hapo Alhamisi baada ya kupitia maeneo yalioathirika zaidi na vurugu hizo za kikabila.

Ethiopia inapakana na Kenya kaskazini na wafugaji wenye silaha hufanya mashambulizi ya wizi wa mifugo kutoka pande zote mbili za mpaka ulio mkubwa kabisa.

Chanzo: DW Swahili